Wajibu logo

A JOURNAL OF SOCIAL & RELIGIOUS CONCERN

Volume 17 No. 3 (2001)

Substance Abuse - Causes and Cures

|
CONTENTS | AFRICANEWS HOMEPAGE |

POEM: WATOTO WA DHIKI

Macho mekundu, kama pilipili, kama dhiki
Puani gundi, rafiki shakiki
Daima pamoja, walalapo, watembeapo
Maisha yao yameunganishwa pamoja
Kwa saruji ya kutojua, umakini.

Hawasikii maneno laini, hawaitwi "kipenzi"
Ulimwengu hauwaimbii wimbo mtamu
Daima wanagombana na chumgu, nzi, kunguru
Kinyanganyiro cha mabaki ya chakula.

Vita vya kupigania pesa nane, vikopo vya gundi
Majeraha usoni, damu, sura ya maisha
Mwendo hoihoi, lugha ya kukokota, ukungu machoni
Safari katika chombo, katika wingu tunduwazi
Sumu katika ubongo, mmomonyoko wa akili
Ulemavu, labda, kujikokota hadi kaburini.

Wanaomba, wanagandama kwa mpita njia
Kama vazi lililonyeshewa mwilini
Wanyakua saa za mikono, vibeti, mikufu
Kwa wepesi, bila kutarajiwa, kama kipanga.

Barabara za miji zinapopata sura mpya, kama mito iliyokauka
Watoto wa gundi wanapigana mieleka mikali, vita
Wanapambana na vikosi vya mbu na kucha za baridi.

Vifo vya asubuhi kabla ya umande kukauka
Kitanzi cha maradhi, msumeno wa madawa ya kulevya
Risasi za wauaji, polisi, milio ya bastola Ngara.

Taifa limelala, linakoroma kama kawaida
Macho ya viongozi hayaoni
Yanalinda viti vya almasi
Mwanachi hajali, anaona watoto wachafu
Haoni Mandela ambaye hatakuwepo, hataongoza
Louis Pasteur ambaye hatakuwa mwanasayansi.

Tuna macho ya bundi, jua linawaka
Tungeona majambazi, Foday Sankoh wa kesho
Hatungeona barabara wazi, bali bomu mbele.

by Kithaka wa Mberia



A JOURNAL OF SOCIAL AND RELIGIOUS CONCERN
Published Quarterly by DR. GERALD J. WANJOHI
Likoni Lane - P .O. Box 32440 - Nairobi - Kenya
Telephone: 254.2.712632/311674/312822


The Online publishing of WAJIBU is by Koinonia Media Centre.


GO TO WAJIBU HOMEPAGE