| 
 
POEM: WATOTO WA DHIKI
 
Macho mekundu, kama pilipili, kama dhikiPuani gundi, rafiki shakiki
 Daima pamoja, walalapo, watembeapo
 Maisha yao yameunganishwa pamoja
 Kwa saruji ya kutojua, umakini.
 
 
Hawasikii maneno laini, hawaitwi "kipenzi"Ulimwengu hauwaimbii wimbo mtamu
 Daima wanagombana na chumgu, nzi, kunguru
 Kinyanganyiro cha mabaki ya chakula.
 
 
Vita vya kupigania pesa nane, vikopo vya gundiMajeraha usoni, damu, sura ya maisha
 Mwendo hoihoi, lugha ya kukokota, ukungu machoni
 Safari katika chombo, katika wingu tunduwazi
 Sumu katika ubongo, mmomonyoko wa akili
 Ulemavu, labda, kujikokota hadi kaburini.
 
 
Wanaomba, wanagandama kwa mpita njia Kama vazi lililonyeshewa mwilini
 Wanyakua saa za mikono, vibeti, mikufu
 Kwa wepesi, bila kutarajiwa, kama kipanga.
 
 
Barabara za miji zinapopata sura mpya, kama mito iliyokaukaWatoto wa gundi wanapigana mieleka mikali, vita
 Wanapambana na vikosi vya mbu na kucha za baridi.
 
 
Vifo vya asubuhi kabla ya umande kukaukaKitanzi cha maradhi, msumeno wa madawa ya kulevya
 Risasi za wauaji, polisi, milio ya bastola Ngara.
 
 
Taifa limelala, linakoroma kama kawaidaMacho ya viongozi hayaoni
 Yanalinda viti vya almasi
 Mwanachi hajali, anaona watoto wachafu
 Haoni Mandela ambaye hatakuwepo, hataongoza
 Louis Pasteur ambaye hatakuwa mwanasayansi.
 
 
Tuna macho ya bundi, jua linawakaTungeona majambazi, Foday Sankoh wa kesho
 Hatungeona barabara wazi, bali bomu mbele.
 
 
 		by Kithaka wa Mberia
  
 
 
  A JOURNAL OF SOCIAL AND RELIGIOUS CONCERN
 Published Quarterly by DR. GERALD J. WANJOHI
 Likoni Lane - P .O. Box 32440 - Nairobi - Kenya
 Telephone: 254.2.712632/311674/312822
 
 
 
The Online publishing of WAJIBU is by Koinonia Media Centre. 
 
 GO TO WAJIBU HOMEPAGE
 |